Jumatano, 1 Juni 2016

Polisi yavuna mamilioni kwa makosa ya barabarani




POLISI mkoani Morogoro kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani imeendesha operesheni maalumu ya kukamataji wa makosa ya usalama barabarani  na kufanikiwa kukamata idadi kubwa ya makosa 9,612 ya magari na pikipiki  katika kipindi cha mwezi Mei, mwaka huu.



Kutokana na idadi hiyo ya makosa ya usalama barabarani, jumla ya Sh milioni 288.3 zimepatikana kutokana na tozo mbalimbali kwa makosa ya magari na pikipiki mkoani Morogoro.



Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema hayo hivi karibuni mjini hapa, kuwa katika oparesheni maalumu ya ukamataji wa makosa ya usalama barabarani ilifanyika kuanzia Mei Mosi hadi mwishoni mwa mwezi huo.



“Polisi mkoa wa Morogoro kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kimeendesha oparesheni maalaumu kwa mwezi Mei na kuweza kukamata jumla ya makosa 9,612 ya magari na pikipiki  kisha kukusanya jumla ya Sh 288,360,000 kutokana na tozo mbalimbali” alisema Kamanda Matei.



Kamanda Matei alitaja aina ya makosa ya magari  ya mwendokasi  ni 2,661, ubovu wa magari 988, kukiuka ratiba 275 , kuzidisha abiria makosa 113,  magari kutokuwa na bima 114 na makosa mengineyo ni 2,908.


Hivi karibuni , Kamanda huyo alisema katika makosa ya usalama barabarani  katika  oparesheni maalumu ya ukamataji wa makosa hayo iliyofanyika Aprili mosi hadi 30, mwaka huu ,  jumla ya makosa 7,838 kwa magari na pikipiki yakikamatwa.



Kutokana na makosa hayo zilikusanywa jumla ya fedha taslimu Sh 235,140,000 kutokana na tozo mbalimbali , ambapo makosa  ya magari yalikuwa  ni mwendo kasi 1,801, ubovu wa magari 909, kukiuka ratiba ya safari 230, kuzidisha abiria 117, kutokuwa na bima 111 na makosa
mengineyo ni 2,110.

ends

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni