Na Shadrack Sagati
Afisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Iringa, Patel
Ngereza
amesema sheria
zinazotumika mahakamani kuwahukumu
wakosaji wa makosa ya barabarani ni dhaifu.
Akizungumza na gazeti hili, Ngereza alisema madereva
wengi wamezoea kulipa faini na wanaona kama ni jambo la kawaida.
“Ipo haja kwa mahakama kuwatoza faini na kuwafunga
kwa makosa yanayofikishwa mahakamani, hii itawaogopesha na kuwafanya wazingatie
sheria,” anasema.
Kuhusu sheria hizo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani anasema mapendekezo yao faini ianzie Sh 100,000 na kifungo kiwe cha
zaidi ya mwaka mmoja.
“Kati ya Machi na April mwaka huu makamanda wa
usalama barabarani tulikutana Morogoro na tukaja na mapendekezo hayo mapya ya
adhabu za makosa ya barabarani, tunaomba wabunge watusaidie kuyapitisha pale
yatakapofikishwa bungeni” anasema.
Anasema takwimu za kimataifa zinaonesha asilimia 51
ya ajali zote duniani zinasababishwa na pikipiki kwahiyo kama nchi inataka iwe
huru na ajali ni lazima sheria za adhabu za makosa ya barabarani ziwe
zinafanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda (CBBI) mkoani Iringa
Hassan Abdul akizungumzia adhabu za hizo, alisema ukubwa wa adhabu hizo unashawishi rushwa na
zinawafanya baadhi ya madereva wasibadilike.
“Rushwa imewafanya baadhi ya madereva hao wawe
watukutu, waendelee kutozingatia sheria za usalama barabarani. Pamoja na
kutozingatia sheria hizo utukutu wa madereva hao umevuka mipaka hadi kwa abiria
wao,” anasema.
Naye Mwenyekiti wa UBBM Makarius Changula ambaye
anakiri kuwahi kukamatwa kwa kuendesha pikipiki isiyo na bima anasema adhabu
kwa madereva wa bodaboda ziangaliwe upya kwani ni kubwa.
“Adhabu ni kubwa sana, zinachochea rushwa na nikiri
baadhi ya askari wa pikipiki, wanapokea sana rushwa kwasababu wanajua hatuwezi
kulipa faini kubwa wanazotutoza, hiyo maana yake ni kwamba tutaendelea kufanya
makosa ya barabarani na kwa kuzingatia madereva wapya wa bodaboda wanazaliwa
kila siku na kuingia barabarani bila kujali sheria zilizopo,” alisema.
Anasema mfumo wa utekelezaji wa sheria za usalama
barabarani na zile za Sumatra ni wa kikandamizi kwasababu umeshindwa
kuzitofautisha bodaboda ambacho ni chombo cha chini kabisa cha moto na vingine
vikubwa zaidi yake.
Changulla anapendekeza faini kwa kosa la barabarani
au lolote linalohusiana na biashara yao iwe Sh 10,000 kwa kosa moja.
Akizungumzia pikipiki zinazokamatwa kwa makosa
yanayohusiana na ukosefu wa stika za Bima, Changulla anasema gharama yake ni Sh
65,000 kwa mwaka, lakini pamoja na wamiliki wengi wa bodaboda hizo kulipa kiasi
hicho kila mwaka, hakuna rekodi inayoonesha kuna msaada wanaopata kutoka katika
makampuni ya Bima pindi wanapopata ajali.
“Pikipiki yako iharibike, dereva au abiria wako
uvunjike au kupata madhara mengine yoyote yale, hakuna fidia yoyote. Sasa
kwanini tuendelee kulipia stika za Bima, malipo hayo ni kwa ajili ya
kumnufaisha nani kama hawana msaada wowote,” anasema.
Anasema katika ofisi ya chama chake, kuna madereva
wanachama wa UBBM zaidi ya 120 waliopata ajali katika mazingira tofauti lakini
hakuna hata mmoja aliyepata fidia toka katika hayo makampuni ya Bima.
ends
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni