Jumatano, 31 Agosti 2016

Madereva wa bodaboda wa Iringa Mjini wakiwa kwenye mafunzo yaliyoendeshwa na chuo cha Future World kupitia programu yao ya Outreach


Sheria dhaifu zinawapa kiburi madereva wa bodaboda



Na Shadrack Sagati
Afisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Iringa, Patel Ngereza
 amesema sheria  zinazotumika mahakamani kuwahukumu wakosaji wa makosa ya barabarani ni dhaifu.

Akizungumza na gazeti hili, Ngereza alisema madereva wengi wamezoea kulipa faini na wanaona kama ni jambo la kawaida.

“Ipo haja kwa mahakama kuwatoza faini na kuwafunga kwa makosa yanayofikishwa mahakamani, hii itawaogopesha na kuwafanya wazingatie sheria,” anasema.

Kuhusu sheria hizo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani anasema mapendekezo yao faini ianzie Sh 100,000 na kifungo kiwe cha zaidi ya mwaka mmoja.

“Kati ya Machi na April mwaka huu makamanda wa usalama barabarani tulikutana Morogoro na tukaja na mapendekezo hayo mapya ya adhabu za makosa ya barabarani, tunaomba wabunge watusaidie kuyapitisha pale yatakapofikishwa bungeni” anasema.

Anasema takwimu za kimataifa zinaonesha asilimia 51 ya ajali zote duniani zinasababishwa na pikipiki kwahiyo kama nchi inataka iwe huru na ajali ni lazima sheria za adhabu za makosa ya barabarani ziwe zinafanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara.


Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda (CBBI) mkoani Iringa Hassan Abdul akizungumzia adhabu za hizo, alisema  ukubwa wa adhabu hizo unashawishi rushwa na zinawafanya baadhi ya madereva wasibadilike.

“Rushwa imewafanya baadhi ya madereva hao wawe watukutu, waendelee kutozingatia sheria za usalama barabarani. Pamoja na kutozingatia sheria hizo utukutu wa madereva hao umevuka mipaka hadi kwa abiria wao,” anasema.


Naye Mwenyekiti wa UBBM Makarius Changula ambaye anakiri kuwahi kukamatwa kwa kuendesha pikipiki isiyo na bima anasema adhabu kwa madereva wa bodaboda ziangaliwe upya kwani ni kubwa.

“Adhabu ni kubwa sana, zinachochea rushwa na nikiri baadhi ya askari wa pikipiki, wanapokea sana rushwa kwasababu wanajua hatuwezi kulipa faini kubwa wanazotutoza, hiyo maana yake ni kwamba tutaendelea kufanya makosa ya barabarani na kwa kuzingatia madereva wapya wa bodaboda wanazaliwa kila siku na kuingia barabarani bila kujali sheria zilizopo,” alisema.

Anasema mfumo wa utekelezaji wa sheria za usalama barabarani na zile za Sumatra ni wa kikandamizi kwasababu umeshindwa kuzitofautisha bodaboda ambacho ni chombo cha chini kabisa cha moto na vingine vikubwa zaidi yake.

Changulla anapendekeza faini kwa kosa la barabarani au lolote linalohusiana na biashara yao iwe Sh 10,000 kwa kosa moja.

Akizungumzia pikipiki zinazokamatwa kwa makosa yanayohusiana na ukosefu wa stika za Bima, Changulla anasema gharama yake ni Sh 65,000 kwa mwaka, lakini pamoja na wamiliki wengi wa bodaboda hizo kulipa kiasi hicho kila mwaka, hakuna rekodi inayoonesha kuna msaada wanaopata kutoka katika makampuni ya Bima pindi wanapopata ajali.

“Pikipiki yako iharibike, dereva au abiria wako uvunjike au kupata madhara mengine yoyote yale, hakuna fidia yoyote. Sasa kwanini tuendelee kulipia stika za Bima, malipo hayo ni kwa ajili ya kumnufaisha nani kama hawana msaada wowote,” anasema.

Anasema katika ofisi ya chama chake, kuna madereva wanachama wa UBBM zaidi ya 120 waliopata ajali katika mazingira tofauti lakini hakuna hata mmoja aliyepata fidia toka katika hayo makampuni ya Bima.

ends

Jumatano, 1 Juni 2016

Madereva bodaboda wananyofowa 'side mirror'



PIKIPIKI nyingi  zinazotoa huduma za usafiri wa abiria katika mji wa Morogoro zimenyofolewa vioo ya upande 'Side Millor’ zinazowezesha dereva kuona kitu kinachokuja nyuma yake akiwa barabarani hali inayohatarisha maisha ya dereva na abiria wa bodaboda.

Mwandishi wa habari hizi  alishuhudia bodaboda nyingi ambaz ziko katika  vituo mbalimbali vya bodaboda , umebaini kuwa kati ya pikipiki 10 zinazoengeshwa , saba hazina  upande kioo,  hali imezifanya  kuwepo kwa  idadi kubwa ya pikipiki zenye mapungufu hayo.

Mmoja wa madereva wa bodaboda, wa mtaa wa Mafisa Jumanne Mayala alisema yeye  ameondoa upande kioo  kwenye pikipiki yake ili kutokana na adha aliyokuwa anaipata anapotaka kupita maeneo yenye barabara nyembamba na kupenya  kati kati ya magari.

“ Upande Kioo ama tunavyoita vioo vya pembeni , zinazuia uwezo wa
kupenya mwenye msongamano wa magari  kutokana na upana wake “ alisema
Mayala.

Mbali na huyo, Dereva mwingine wa  bodaboda  wa mtaa wa  Uguu , Kata
ya Uwanja wa Taifa aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Juma , alisema
yenye aliondoa ili  kupata urahisi wa kuingiza pikipiki ndani ya chumba la kulaza kutokana na baadhi ya milango upana wake kuwa mdogo.

Juma alisema madereva wengi wa  pikipiki za biashara maengesho yao ni
kwenye makazi wanakoishi.

Naye Dereva wa bodaboda mkazi wa Mwembesongo aliyejitambulisha kwa
jina la Charles  Frank , alisema  upande kioo  katika pikipiki  vina
umuhimu wake  katika kusaidia usalama wa dereva na abiria .

Hivyo alisema kuondoa  Upande Kioo  mwa pikipiki ni  makosa ya sheria
ya usalama barabarani na  pia ni jambo hatarishi  kwa mwendeshaji
kutokuwa salama akiwa barabarani.

“ Mara nyingi  upande kioo  vinasaidika kuona nyuma kitugani kinakuja
na kipo umbali gani na pia kusadia wakati wa kutaka kuingia  upande
mwingine wa barabara  bila kugeuka nyuma “ alisema Frank .

Kwa upande wake, Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa
Morogoro, Boniface Mbao , alisema kuwa, kuondoa  upande kioo ‘ Side
Millor ‘ katika  pikipiki ni kosa kisheria na kwamba  opereshani
maalumu inaendelea kufanyika kuhusiana  makosa hayo .

Mbao alisema ,  pikipiki za aina hiyo  zinapokamatwa zinahesabika
zinaendeshwa barabarani zikiwa na ubovu  na wakosaji wa makosa hayo
watatozwa adhabu kwa mujibu wa sheria za makosa ya usalama barabarani.

Kutokana na pikipiki kutozingatia sheria za usalama barabarani, mwezi Mei katika operesheni iliyofanywa na polisi wamekamata waendesha pikipiki 1,189 kwa kutoava kofia ngumu, 248 wanaendesha bila bima, 168 hawana leseni na makosa mngine 955.

Mwisho.

Polisi yavuna mamilioni kwa makosa ya barabarani




POLISI mkoani Morogoro kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani imeendesha operesheni maalumu ya kukamataji wa makosa ya usalama barabarani  na kufanikiwa kukamata idadi kubwa ya makosa 9,612 ya magari na pikipiki  katika kipindi cha mwezi Mei, mwaka huu.



Kutokana na idadi hiyo ya makosa ya usalama barabarani, jumla ya Sh milioni 288.3 zimepatikana kutokana na tozo mbalimbali kwa makosa ya magari na pikipiki mkoani Morogoro.



Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema hayo hivi karibuni mjini hapa, kuwa katika oparesheni maalumu ya ukamataji wa makosa ya usalama barabarani ilifanyika kuanzia Mei Mosi hadi mwishoni mwa mwezi huo.



“Polisi mkoa wa Morogoro kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kimeendesha oparesheni maalaumu kwa mwezi Mei na kuweza kukamata jumla ya makosa 9,612 ya magari na pikipiki  kisha kukusanya jumla ya Sh 288,360,000 kutokana na tozo mbalimbali” alisema Kamanda Matei.



Kamanda Matei alitaja aina ya makosa ya magari  ya mwendokasi  ni 2,661, ubovu wa magari 988, kukiuka ratiba 275 , kuzidisha abiria makosa 113,  magari kutokuwa na bima 114 na makosa mengineyo ni 2,908.


Hivi karibuni , Kamanda huyo alisema katika makosa ya usalama barabarani  katika  oparesheni maalumu ya ukamataji wa makosa hayo iliyofanyika Aprili mosi hadi 30, mwaka huu ,  jumla ya makosa 7,838 kwa magari na pikipiki yakikamatwa.



Kutokana na makosa hayo zilikusanywa jumla ya fedha taslimu Sh 235,140,000 kutokana na tozo mbalimbali , ambapo makosa  ya magari yalikuwa  ni mwendo kasi 1,801, ubovu wa magari 909, kukiuka ratiba ya safari 230, kuzidisha abiria 117, kutokuwa na bima 111 na makosa
mengineyo ni 2,110.

ends

Ijumaa, 27 Mei 2016

Kamanda wa Usalama Barabarani mkoa wa Morogoro Mrakibu wa Polisi Boniface Mbao akizungumza na mwandishi wa gazeti la Habarileo Shadrack Sagati kuhusu mambo mbalimbali ya usalama barabarani.